Serikali imeibuka kidedea kwenye kesi iliyokuwa ikiendeshwa katika Baraza la Kimataifa la Biashara (International Chamber of Commerce-ICC) dhidi ya Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.
Uamuzi wa kuipa Tanzania ushindi katika Shauri la Usuluhishi Na. 2682/AZO baina ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency-PBPA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Kampuni hiyo, umetolewa na ICC Machi 6, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, shauri hilo lilifunguliwa baada ya Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kushindwa kusambaza mafuta kwa mujibu wa mkataba uliotokana na zabuni Na. PBPA/CPP/PMC/C3-KOJI/02/2021 wa Januari 5, 2021 kwa ajili ya kuleta nchini mafuta, metriki za ujazo 36,192. Mafuta hayo yalipaswa kupokelewa nchini kuanzia Februari 27, 2021 hadi Machi 1, 2021.
Kwa upande wa Serikali, taarifa inaonesha jopo la utetezi liliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akishirikiana na mawakili wengine kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Katika uamuzi wake, Baraza limetamka bayana kuwa Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC ilivunja mkataba na hivyo likaiamuru kurejesha fedha kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), dola za Marekani milioni 9.7 pamoja na riba kabla ya tuzo (pre-award interest) ya asilimia 7.67 kuanzia Mei 18, 2021 hadi Novemba, 2023; kwa kuvunja mkataba na kushindwa kuleta mafuta nchini.
Taarifa inaonesha kwamba mbali na kurejesha kitita hicho cha fedha, kampuni hiyo imeamriwa pia kuilipa PBPA dola za Marekani milioni 1.14 kama adhabu ya kuharibu mfumo wa ununuzi wa mafuta. Kampuni hiyo pia inatakiwa kuilipa PBPA dola za Marekani 882,000.00 kufidia gharama ilizotumia kuendesha kesi kwenye baraza na pia kulipa gharama za kesi zinazofikia Dola za Marekani 818,285,700.00.
Taarifa inasema kampuni hiyo pia inatakiwa kuilipa riba baada ya tuzo (post award interest) asilimia 7.67 kuanzia uamuzi ulipotolewa Machi 6, 2024 hadi itakapokamilisha malipo yote inayodaiwa.
“Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kusimamia na kuendesha mashauri ya kimataifa kwa weledi na kulinda maslahi mapana ya Taifa letu,” imesema taarifa hiyo.