Serikali yafuta tozo 42 zao la Kahawa

0
233

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuondoa tozo 42 kati ya 47 ambazo walikuwa wanatozwa wakulima wa Kahawa wa mkoa wa Kagera hadi kufikia tozo 5 tu ambazo itakuwa ni jumla ya Shilingi 267 kwa kila kilo ya kahawa, kutoka shilingi 830 za awali.

Waziri Mkuu ametoa maamuzi hayo kufuatia tume maalum aliyoiunda ili kupitia utaratibu na mfumo wa uendeshaji wa vyama vya ushirika wa zao la kahawa mkoani humo.

Pia, Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vikuu vya ushirika kuacha tabia ya kukopa pesa benki kwa ajili ya kununua kahawa kwa wakulima.

Amesema kuanzia sasa mauzo ya kahawa katika Mkoa wa Kagera yatafanyika kwa njia ya mnada. “Mnada huo utafanyika kwenye ngazi ya vyama vya msingi.”

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema baadhi ya vyama vya ushirika vimekuwa vikiwaumiza wakulima wa kahawa kwa kuwaongezea tozo zisizokuwa na tija.

Waziri Bashe amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa kugawa miche ya kutosha ya kahawa kwa wakulima ili ilete tija na kuwaongezea kipato.

Amesema ili kuhakikisha maafisa ugani wanatekeleza majukumu yao ipasavyo Wizara imeandaa utaratibu wa kutoa usafiri pamoja na vifaa vya kupimia udongo.