Serikali yafuta maonesho ya Nanenane 2021

0
303

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ametangaza kusitisha shughuli zote za maonesho ya Nanenane zilizokuwa zifanyike mwaka huu mkoani Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, amesema fedha zote za umma bila kujali ni za wizara gani, zisitumike kwenye shughuli hizo.

“Tunawasiliana na wizara nyingine na wadau kwamba fedha hizo tuzielekeze katika kuendeleza shughuli za ugani,” amesema waziri huyo.

Amesema hivi karibuni wamekuwa na kikao na maofisa kilimo wa mikoa, kujadiliana kuhusiana na changamoto ambazo baadhi zinahitaji uwezeshwaji kifedha ili wazitatue.

“Tuna maofisa tumewaajiri hadi ngazi ya kata kwa ajili ya kilimo, lakini changamoto tulizozizungumza wakati ule zinahitaji na sisi kuwawezesha vilevile, kwa sababu hatuna haja ya kuweka ofisa kule lakini hatuwawezesha wao kuwasaidia wananchi,” amesema.

Ameongeza kuna wakulima hawajui wanapataje huduma za ugani hivyo anawasiliana na wizara nyingine ambazo ni wadau kwenye shughuli hizo kwamba fedha yote iliyokuwa itumike kwa ajili ya shughuli za Nanenane mwaka huu ipelekwe katika shughuli za kuimarisha ugani.