Serikali yadhibiti wizi wa mafuta bandarini

0
159

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla leo Agosti 20, 2021 ameshuhudia na kukagua kifaa cha kisasa cha kubaini wizi na upotevu wa mafuta ghafi (radio detector) kutoka bomba kuu la kupokea mafuta kutoka kwenye meli kuelekea kwa wafanyabiashara ambapo kifaa hicho kinatarajiwa kuanza zoezi la ukaguzi muda wowote kuanzia leo.

Upatikanaji wa kifaa hicho ni kufuatia maelekezo aliyotoa Makalla kwa TPA baada ya kuunda kamati ya ufuatiliaji upotevu wa mafuta ambapo miongoni mwa mapendekezo ya kamati ilikuwa ni ununuzi wa kifaa cha kudhibiti wizi wa mafuta bandarini.

Aidha Makalla amewahakikishia wafanyabiashara wa mafuta kuwa Serikali imejidhatiti kumaliza kabisa tatizo la upotevu wa mafuta na anashukuru kuona hadi sasa kumekuwa na matokeo mazuri.

Katika ziara yake, Makalla pia ametembelea ujenzi wa barabara za kuingia na kutoka bandarini na upanuzi wa eneo la kushusha na kupakia mizigo ambapo ameipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa mapinduzi makubwa ya maboresho ya huduma kwa wananchi.