Serikali yabanwa ongezeko la bidhaa feki

0
257

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Juliana Masaburi ameitaka serikali kujitathmini namna ambavyo inashughulikia udhibiti wa bidhaa feki ambazo zinazalishwa hapa nchini ama kuingizwa kutoka nje ya nchi.

Akiuliza maswali mawili ya nyongeza wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma, Masaburi amesema serikali ni lazima iwe na udhibiti wa bidhaa feki za vyakula, vipodozi na dawa kwa kutumia mamlaka sahihi tofauti na ilivyo sasa.

“Mheshimiwa Spika kwa sasa TBS ndio wanasimamia udhibiti wa vyakula, dawa na vipodozi feki, kwa nini serikali isirudishe usimamizi kwa wizara ya Afya ambapo kuna wataalamu ambao wamesomea udhibiti wa bidhaa hizo?” ameuliza Masaburi

Akijibu maswali hayo Naibu waziri wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema, serikali itakaa na kuona namna ya kuhamisha udhibiti wa bidhaa hizo kwenye mamlaka zingine kwa ajili ya udhibiti zaidi.