Serikali imesema imebaini uwepo wa ongezeko la watu wenye dalili za homa, kukohoa, mafua, kubanwa kifua na maumivu ya mwili kwa kipindi cha Desemba 2021 hadi Machi 25, 2022.
Ongezeko hilo limekuwa likitokea katika kipindi cha mwishoni na mwanzoni mwa mwaka kwa miaka mitatu mfululizo ambapo imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.
Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichwale imeeleza kuwa Serikali imebaini uwepo wa kirusi cha Infuenza ambapo kati ya sampuli 1,843 zilizopimwa kwa kipindi cha 12 Desemba 2021 hadi 13 Machi 2022 sampuli 53 ambayo ni sawa na asilimia tatu zilionekana kuwa na virusi vya Influenza A vinavyosababisha mafua makali na nimonia.
“Kirusi hiki kimekuwepo hapa nchini kwa muda mrefu na siyo kirusi kipya, kiwango cha maambukizi ya kirusi hiki kinaonesha kupungua ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kilikuwa cha wastani wa asilimia 5 hadi 6.
Takwimu zilizokusanywa zinaonesha ongezeko la wagonjwa wenye dalili za homa, kukohoa, mafua, kubanwa kifua na maumivu ya mwili tangu Desemba 2021 hadi 25 Machi 2022, ingawa takwimu hizo zilionesha kupungua kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka uliopita” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika ufuatiliaji huo sampuli 123 zilichukuliwa kwa watoto wenye dalili hizo ambapo sampuli 16 kati ya 123 ambayo ni sawa na asilimia 13 zilikuwa na virusi vya mafua ya influenza A.