Serikali yaagiza shule kupelekewa walimu

0
873

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa  muda wa siku mbili kwa Kaimu Afisa Elimu anayeshughulikia elimu ya msingi wilayani Muleba  mkoani Kagera, – Bukuru Malembo awe amepeleka walimu wawili katika shule ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kwa kuwa haina mwalimu hata mmoja.

Shule hiyo yenye madarasa wawili na ofisi moja ya mwalimu, ina jumla wanafunzi 216 wa darasa la awali hadi la nne.

Shule hiyo ilijengwa na wananchi ambapo kwa sasa wanafunzi wake wanafundishwa na mwananchi mmoja aliyeamua kujitolea ili kuwapunguzia adha watoto ya kutembea umbali wa kilomita 16 kwenda kusoma katika shule ya kijiji cha Kiteme.

Waziri Mkuu  Majaliwa ametoa muda huo baada ya wanafunzi wa shule hiyo ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya bango wakati akizungumza na wakazi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara.

“Haiwezekani watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano wakatembea umbali wa kilomita 16 kwenda shule wakati katika kitongoji chao kuna shule yenye madarasa mawili na chumba kimoja cha ofisi ya mwalimu na Afisa Elimu hadi sasa hajapeleka walimu na kumuachia mwalimu Benson Bukerebe, kijana ambaye si mwalimu ila anajitolea kufundisha akifundisha wanafunzi hao peke yake”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa  amemuagiza kaimu Afisa Elimu huyo  anayeshughulikia elimu ya msingi wilayani Muleba  ahakikishe ifikapo Oktoba Kumi mwaka huu saa nne asubuhi awe ameshawapeleka walimu hao wawili katika shule hiyo ya msingi ili waweze kuwafundisha wanafunzi.

Pia amemtaka mkuu wa wilaya ya Muleba, -Mhandisi Richard Ruyango awasilishe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ofisini kwake.

Kwa upande wake, Benson Bukerebe  mwenye umri wa miaka 29,  maarufu kama mwalimu Benson amesema kuwa yeye kitaaluma si mwalimu bali ni mhitimu wa kidato cha nne na aliamua kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi hao kwa kuwa alikuwa akiwahurumia kwa sababu baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 16 hadi iliko shule ya msingi ya Kiteme.

Amesema kuwa kwa muda wote huo ameweza kumudu kuwafundisha wanafunzi hao kwa kutumia vitabu vya kuazima kutoka shule mbalimbali za msingi, lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji chao cha Rwenzige wanapata fursa ya elimu ambayo ni haki yao ya msingi.