Serikali yaagiza kuwezeshwa Wabunifu wachanga

0
235

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi na mamlaka ambazo zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga zihakikishe zinawawezesha kufanya ubunifu na uvumbuzi wao kibiashara.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akifunga maonesho ya mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri.
 
Amesema kuwa uendelezwaji wa wabunifu na wavumbuzi ufanyike kwa kasi na ufanisi mkubwa, ili kuhakikisha matunda ya jitihada zinazofanywa na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwaibua na kuwatambua wabunifu wachanga zinazaa matunda.
 
“Taasisi za sayansi na teknolojia, vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo na mamlaka mbalimbali kama SIDO, VETA na DON BOSCO ambazo kwa namna moja ama nyingine zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga ziwasaidie kufanya ubunifu na uvumbuzi wao kibiashara,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Pia amezitaka taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti na maendeleo zishirikiane na sekta binafsi hasa ya viwanda, ziweke utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na zihamasishe matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
 
Amesema nia ya Serikali ni kuona ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia zinazozalishwa na wabunifu wachanga unatoa mchango mkubwa katika kuzalisha ajira mpya, kuongeza kipato kwa wabunifu na kuchangia katika pato la Taifa.
 
Akizungumzia mitaala ya elimu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ni vema iandaliwe kwa namna ambayo itawawezesha wahitimu kuwa wabunifu na hatimaye waweze kutumia ubunifu huo kujitengenezea ajira zao  na ikiwezekana wawaajiri wengine.