Serikali yaagiza kusambazwa kwa wataalamu wa afya wa kutosha

0
278

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupeleka wataalamu wa kutosha katika maeneo yenye mahitaji makubwa ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandarini ili waweze kuongeza nguvu katika kuzuia maambuzi ya virusi vya corona.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akiongoza kikao cha kamati ya kitaifa ya kukabiliana na virusi vya corona, kikao kilichohusisha wajumbe kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Pia ameiagiza wizara hiyo ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini wanapimwa na wanafuatiliwa, ili kujua historia zao za safari katika kipindi cha siku 14, lengo likiwa ni kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa Watendaji wote waliopewa dhamana ya kuratibu zoezi la kupeleka watu walio kwenye karantini, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wahakikishe wahusika wanafika kwenye hoteli walizochagua na kwamba serikali inafanya utaratibu wa kutenga maeneo ambayo watu watakuwa wanakaa bila gharama na yatakuwa na huduma zote muhimu.

Machi 23 mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa aliunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona nchini, ikiwa ni pamoja na kamati hiyo ya kitaifa inayoongozwa na yeye mwenyewe.