Serikali yaagiza elimu ya moto kutolewa shuleni

0
219

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, David Silinde ametoa rai kwa shule zote za bweni nchini kuweka vizima moto (fire extinguishers) na vitambuzi vya moto (smoke detector) ili kukabiliana na ajali za moto pindi unapoanza katika mabweni ili kuokoa uhai wa wanafunzi na mali zao.

Ametoa rai hiyo mara baada ya kutembelea Shule ya Sekondari Geita ambayo iliunguzwa moto mara tatu na baadhi ya wanafunzi ndani ya siku saba na kutaka elimu ya kujikinga na majanga ya moto itolewe na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini ili kunusuru mali nyingi za shule na uhai wa wanafunzi.

Aidha, Silinde ametaka wanafunzi wote watakaobainika bila kuonewa kuwa wameshiriki katika kuunguza mali za shule hiyo hatua kali za kinidhamu zichukuliwe juu yao, wazazi wao watahusika kuzirudishia gharama za mali zilizoharibika ili iwe fundisho kwa wanafunzi wengine. Amewaagiza walimu wa shule hiyo kukazania nidhamu shuleni hapo baada ya kuonekana nidhamu ya wanafunzi kua chini.

Ameongeza kuwa, kwa sasa vipindi vya dini viwe vya lazima kufundishwa katika shule zote licha ya kutokufanya mtihani, kwani inaonekana wanafunzi ambao wanahofu ya Mungu hawawezi fanya utovu wa nidhamu, kuchoma mali za shule.

Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo, Isaya Busagwe amesema shule yao ilikumbwa na ajali ya moto Julai 5, 6 na 14 katika miundombinu ya madarasa ya kidato cha sita na bweni lenye wanafunzi 80 viliathiriwa vibaya na moto, na mpaka sasa wanafunzi tisa wamebainika kuhusika na matukio hayo.