Serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 42 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ziwa Viktoria, ili kuongeza tija ya utoaji huduma za usafiri wa majini kwa watu na mali zao.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Meli Tanzania (MSCL) Eric Hamissi ametoa taarifa hiyo wakati akielezea mafanikio ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani kwa mkoa wa Mwanza.
Hamissi amesema ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu unaendelea vizuri na tayari meli hiyo imefikia hatua ya kushushwa kwenye maji, hatua ambayo ni muhimu katika ujenzi wa meli.
Ameongeza kuwa kwa hivi sasa Serikali pia inaendelea na ukarabati wa meli kubwa ya mizigo inayoweza kubeba shehena kubwa ya mizigo katika ziwa Viktoria ambapo serikali imetumia shilingi Bilioni 19 kwa ukarabati huo.