Serikali kutumia trilioni 36.3 mwaka ujao wa fedha

0
212


Serikali inatarajia kukusanya na kutumia shilingi trilioni 36.3 katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022,  ikiwa ni ongezeko la asilimia nne ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango,  wakati akiwasilisha mpango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Amesema kati ya fedha hizo za ndani zinatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26 sawa na asilimia 71.8 ya bajeti yote, misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo shilingi trilioni 2.9, mikopo ya ndani shilingi trilioni 5 na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 2.4.

Kwa mujibu wa Dkt Mpango, kati ya fedha hizo zinazotarajiwa kukusanywa na kutumiwa, shilingi trilioni 23 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 63 ya bajeti yote.