Serikali kutoa vitambulisho vipya vya Wamachinga vilivyoboreshwa

0
206

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kutoa vitambulisho vipya vya wamachinga vilivyofanyiwa maboresho ambavyo vitakuwa na picha ya muhusika na baadhi ya kumbukumbu binafsi zitakazomtambulisha na kumuwezesha kupewa huduma katika maeneo mbalimbali zikiwemo na taasisi za kifedha.

Amesema vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa Aprili Mosi mwaka huu, hivyo amewataka wakuu wa mikoa na wilaya wahakikishe wamachinga wanaendelea kufanya shughuli zao bila ya bugudha katika kipindi hiki ambacho muda wa matumizi ya vitambulisho vyao umekwisha.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa vitambulisho hivyo vitakuwa na picha ya mhusika, hivyo haitawezekana kutumiwa na mtu mwingine na pia vitadumu kwa miaka miwili hadi mitatu tofauti na vya sasa ambavyo vilikuwa vya mwaka mmoja.

“Serikali kupitia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kutoa vitambulisho rasmi ambayo vitawatambulisha popote na kupata huduma muhimu kama vile kutambulika na taasisi za fedha na maeneo muhimu.”

Kadhalika, amewaagiza viongozi wa wamachinga wahakikishe wanakuwa na takwimu sahihi idadi ya Wamachinga ili iwe rahisi kuwahudumia. “Tuwe na kanzidata ya wamachinga itarahisisha mawasiliano ndani ya Shirikisho la Wamachinga na Serikali. Mkijiunga pamoja na kutambuliwa ni rahisi kwa taasisi za kifedha kuwafikia na kuwapatia huduma za mikopo itakayowawezesha kukuza mitaji yenu.”

Alisema Serikali imedhamiria kumhudumia na kumtumikia kila mwananchi wakiwemo Wamachinga kwa lengo la kuwawezesha kukuza biashara zao na kujikwamua kiuchumi, hivyo aliwataka wafanye kazi kwa bidii.