Serikali kutoa maelezo kuhusu uendeshaji wa uwanja wa KIA

0
298

Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amemtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa kupeleka bungeni majibu ya kujitosheleza Novemba 5, 2022 kuhusu uendeshaji wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Dkt. Tulia ametoa agizo hilo leo bungeni jijini Dodoma baada ya kuibuka mkanganyiko juu ya uendeshaji wa uwanja huo ambao kwa mujibu wa Profesa Mbarawa unaendeshwa na kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji wa uwanja wa Ndege Kilimanjaro (KADCO), lakini kisheria Spika amesema kampuni hiyo haitakiwi kuwepo.

Akitoa hoja zake bungeni Profesa Mbarawa amesema, kabla ya mwaka 2009 KIA ilikuwa na wanahisa wanne ambapo Serikali ilikuwa inamilikia asilimia 24, MacDonald kutoka Uingereza aliyekuwa anamiliki asilimia 41.4, South Africa Infrastructure Fund iliyokuwa inamiliki asilimia 30 na Inter-Consult Ltd ya Tanzania iliyokuwa inamilikia asilimia 4.6.

Baada ya mwaka huo Serikali ilinunua hisa za wanahisa wote hivyo kumiliki uwanja huo kwa asilimia 100 chini ya kampuni ya KADCO (iliyo chini ya wizara) kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010.

Hata hivyo, Spika Tulia amehoji, Serikali ilipowanunua wanahisa wengine ilipata umiliki wa uwanja huo kwa asilimia 100, sasa mkataba unaozungumziwa sasa unatoka wapi? .

“Kamati wanazungumzia mkataba, kwamba mkataba unaisha Juni 2023. Ni mkataba gani?. Kwa sababu KADCO kimsingi ile iliyokuwepo awali ni kwamba haipo, kisheria. Kama haipo, haya mazungumzo ya mkataba yanatokana na nini?.” amehoji Spika

Pia amehoji kwanini Serikali iliponunua hisa haikurejesha uwanja huo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kama ulivyo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Suala la tatu alilohoji ni, kwa vile KADCO ndio wanalipa fedha Serikalini, na sio Serikali inajilipa fedha, hiyo KADCO imezishikilia wapi hizo fedha, kisha ndio iilipe Serikali? .

Baada ya majibu ya waziri kutojitosheleza, Spika Tulia amesema Waziri Mbarawa atapewa nafasi Jumamosi ili atoe ufafanuzi ambao utalisaidia bunge wakati likitoa maazimio kwa Serikali, baada ya kupitia taarifa za kamati za bunge.