Serikali kutathmini kupanda bei ya mafuta

0
225

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama za maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
 
“Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi,”  amesema.
 
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Mei 5, 2022) katika kikao kilichofanyika usiku kwenye  ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.
         
Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.
 
Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, January Makamba, Makatibu Wakuu, pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).