Serikali imesema imesikia hoja mbalimbali zilizotolewa na Wananchi kuhusu tozo za miamala ya simu, na inalifanyia kazi jambo hilo.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema viongozi wakuu akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan tayari wametoa maelekezo ya namna ya kushughulikia jambo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limeonekana kuleta malalamiko miongoni mwa Wananchi.
Amesema yeye pamoja na Waziri mwenzake wa wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika wameanza kushughulikia malalamiko hayo ya tozo kwenye miamala ya simu.
Kwa mujibu wa Dkt. Nchemba, kesho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye atakutana na Wadau mbalimbali, ili kujadili changamoto zilizojitokeza katika tozo hizo.
Amewataka Watanzania wote kuendelea kuwa watulivu wakati jambo hilo linashughulikiwa.
Tarehe 15 mwezi huu, kampuni mbalimbali za simu nchini zilianza kutoza tozo mpya za miamala ya simu.