Serikali kupitia upya kanuni za uvuvi za mwaka 2020

0
386

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kufuatia changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa marekebisho ya kanuni za uvuvi za mwaka 2020 serikali imeazimia kuzipitia upya ili ziendane na mahitaji ya sasa.

Ndaki ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya zana za uvuvi katika maji yote nchini.

Amesema hivi karibuni Wizara imepokea maoni na changamoto mbalimbali kutoka kwa wadau wa sekta ya uvuvi kutoka Ukanda wa Bahari, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria kuhusiana na marekebisho ya kanuni ya uvuvi ya mwaka 2020 katika baadhi ya vipengele.

Ndaki alisema kuwa maeneo ambayo yameonesha kuwa na changamoto nyingi ni katika uvuvi wa kutumia nyavu za mtando (Ring net) wakati wa mchana katika ukanda wa Bahari ya Hindi, utaratibu wa kupima ukubwa wa macho ya nyavu kwa kutumia kipimo kilichoainishwa katika kanuni kinachofahamika kama Mesh Gauge na uvuvi wa Dagaa wakati wa mbalamwezi.

Kufuatia changamoto hizo, ametoa maelekezo kuwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ifanye utafiti kuhusu uvuvi wa kutumia nyavu za mtando na iwasilishe taarifa kwa Waziri huyo ndani ya siku kumi na nne (14) ili serikali iweze kutoa maelekezo.

Kuhusu utaratibu wa kipimo cha ukubwa wa nyavu, waziri amesema kuwa watashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na watatoa maelekezo ni kipimo gani kitumike lakini kwa sasa utaratibu wa kupima nyavu uendelee kama ilivyokuwa awali kwa kutumia kipimo cha Venier Calliper.

Pia, Ndaki amewaagiza wataalamu wa wizara kutoa haraka mwongozo kuhusu uvuvi wa Dagaa wakati wa mbalamwezi ili kuondoa sintofahamu iliyopo sasa ya wakati gani hasa uvuvi huo ufanyike.

Aidha, Ndaki ameongeza kwa kusema kuwa wizara yake itapitia upya marekebisho ya kanuni zote za uvuvi na kuharakisha marekebisho ya kanuni nzima ya Mwaka 2009 ili iendane na wakati.