Serikali kupanua kiwanja cha ndege cha Tanga

0
87

Serikali imesema iko katika hatua za mwisho za kuanza upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Tanga, kwa kuboresha miundombinu yake ili kuendelea kufungua biashara katika mkoa huo.

Akizungumza jijini Tanga, Naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema nia ya serikali ni kuufanya mkoa wa Tanga kukua zaidi kibiashara hasa kwa kuzingatia kuna miradi mikubwa inayotekelezwa mkoani humo ambayo kukamilika kwake kunahitaji njia zote za usafiri.

“Mkoa wa Tanga kwa sasa kuna miradi mikubwa inayotekelezwa mfano upanuzi wa bandari, pia kuna miradi itakayotekelezwa kama ujenzi wa bomba la mafuta likalojengwa kuelekea nchini Uganda, hivyo lazima tuhakikishe miundombinu wezeshi inakuwepo mapema.” amesema Naibu Waziri Mwakibete

Ameutaka uongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Tanga na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuhakikisha wanakaa pamoja kwenye kila hatua ili kupunguza changamoto za kiutendaji ambazo zinaweza kujitokeza mara mradi utakapokamilika.

Kwa upande wake Meneja wa kiwanja cha ndege cha Tanga, Mussa Mchola amesema, kiwanja hicho kwa sasa kinahudumia ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya watano na 12 za ratiba na zisizo za ratiba.