Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kwamba serikali itagharamia gharama za wananchi wote wanatakaokuwa tayari kuhama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari.
Waziri Mkuu amesema hayo wakati akitoa hoja ya kuahirisha bunge jijini Dodoma na kueleza zaidi kwamba suala la kulinda mazingira ni la Watanzania wote.
Kiongozi huyo ambaye amefanya mazungumzo na wakazi wa eneo hilo hivi karibuni amewasihi wale wote walioko tayari kuhama wasikwamishwe na watu wengine.
Amewataka wanaotaka kuhama kujiandikisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mkuu wa Wilaya ya Karatu na Mhifadhi Mkuu.
Ameeleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na watu wote kulinda mazingira ya eneo hilo na maeneo mengine nchini.
Akitilia mkazo suala hilo, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa huo ndio uamuzi wa sasa wa serikali, na kuwataka wananchi kupuuza uzushi kuwa bunge limetunga kanuni za kuwaondoa wananchi hao.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameahirisha bunge hadi Aprili 5, 2022 saa tatu asubuhi.