Serikali kuleta suluhu ya Mawasiliano Tabora Vijijini

0
202

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew, amesema huduma za Mawasiliano maeneo ya Tabora vijijini zitaendelea kuimarika endapo wakazi wa maeneo hayo watashiriki kikamilifu katika zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi pamoja na Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika
Agosti, 2022.

Mhandisi Kundo ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa upatikanaji huduma za Mawasiliano, miradi ya UCSAF katika maeneo ya pembezoni mwa Tabora wakati alipotembelea kata ya Itetemia kitongoji cha Kipalapala na kukagua hatua iliyofikia ujenzi wa mnara wa Mawasiliano kutoka kampuni ya Halotel na kumalizia ziara yake katika vitongoji vya Ifucha, Kipalapala na Kakolamabapo alipoenda kutoa elimu juu ya mfumo huo pamoja na Sensa ya Watu na Makazi ya 2022.

Amesema kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania Bilioni 28
ambacho kinaenda kutumika katika utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi na kuwataka wananchi wa sehemu hizo kushiriki kikamilifu katika kutimiza zoezi hilo pamoja na kuhesabiwa ili iwe rahisi kwa Serikali kupeleka maendeleo katika maeneo yao kwa kujua idadi husika ya watu wanaoishi mahala hapo ikiwemo kuwapatia huduma bora za Mawasiliano kwa kuwekewa minara ya simu yenye ukubwa unao lingana na idadi ya watu hao.

“Mheshimiwa Rais kwa kulitambua hilo tayari ameshaidhinisha kiasi cha Bilioni 28 za Kitanzania kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa Anwani za Makazi kwa kila Mtanzania hasa wananchi wa Kakola, Mheshimiwa Rais anafahamu mpo basi jitokezeni na mkahamasishe na wenzenu.”-amesema Mhandisi Kundo.