Naibu Waziri Mifungo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ili kuimaliza.
Ulega ambaye ni Mbunge wa Mkuranga mkoani Pwani ameyasema hayo wakati wa mkutano wake na wananchi alipofanya ziara kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.
Akijibu maswali ya wananchi amesema kumekuwa na migogoro kati ya wafugaji na wakulima maeneo mengi hapa nchini na kuahidi kulishughulikia haraka kabla ya maafa makubwa kutokea
“Katika bajeti ya mwaka huu wa 2021/2022 Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na sisi watu wa Mkuranga tumekumbukwa kwa kupata pesa nyingi za kuboresha miundombinu na sekta nyingine kama vile elimu, afya na mengine mengi, sisi kazi yetu ni kumwombea Rais wetu na kuchapa kazi tu,” amesisitiza Ulega