Serikali ya imejipanga kiuhakikisha kuwa anuai za jamii zinajumuishwa kwenye TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro wakati akifungua kikao cha wadau wa taasisi za Serikali na anuai za jamii ikiwemo watu wenye ulemavu, vijana, wazee na wanawake kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano uwanja wa Ndege Dodoma chenye lengo la kuhakikisha kuwa anuai hizo za jamii zinajumuishwa kwenye TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili makundi hayo maalum yaweze kutumia na kunufaika na TEHAMA nchini.
Dkt. Ndumbaro amesema kutokana na mabadiliko ya TEHAMA duniani ambapo imepelekea huduma nyingi kutolewa kupitia TEHAMA, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itahakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa na kumfikia kila mwanachi kwa wakati ili kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 kwa kutambua na kukusanya mahitaji ya anuai za jamii.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Ernest Kimaya, ameishukuru Serikali kwa kuwaalika na ameiomba iangalie uwezekano wa kuongeza vifaa rafiki vya TEHAMA na matumizi yake kwa wananchi hususani kwa anuai za jamii ikiwa ni pamoja na kushirikisha watendaji wa anuai za jamii katika ngazi za kata hadi taifa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI itumike kufikisha na kutekeleza hilo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakati akifunga kikao hicho amesema kuwa mabadiliko ya teknolojia yanagusa maisha ya kila siku katika nyanja za kiuchumi na kijamii ambapo Serikali kwa kutambua hilo imeweka sera, sheria, kanuni pamoja na kujenga miundombinu ya TEHAMA, kutoa huduma za mawasiliano ili kuhakikisha kuwa wananchi wote pamoja na anuai za jamii zinajumuishwa na kushirikishwa katika TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali.