Serikali kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) ikishirikiana na Serikali ya China inatarajia kujenga hospitali kubwa ya moyo katika eneo la Mloganzila ambapo hatua za awali za mchakato wa ujenzi zimekamilika.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohammed Janabi ameeleza kuwa katika miaka minne ya serikali ya awamu ya tano taasisi hiyo imepanua huduma zake na kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa kiwango cha kimataifa.
“Katika kipindi cha miaka minne wagonjwa waliopatiwa huduma ni 300,836 ambao walitibiwa na kurudi nyumbani na wagonjwa 14,960 ambao walilazwa kwa ajili ya kupata matibabu zaidi, na mahitaji yanazidi kuongezeka hata kutoka katika nchi jiranii,” amesema Prof. Janabi.
Janabi amebainisha kuwa mahitaji ya ujenzi wa hospitali kubwa ya Mloganzila yanatokana na kuwepo kwa wagonjwa wengi nje ya nchi ambao wamekuwa wakija kupata matibabu kwa hiyo uwepo wa hospitali hiyo kutaimarisha utoaji huduma za matibabu ya moyo hapa nchini.
Katika kipindi cha miaka minne JKCI imeweza kufanyia upasuaji mkubwa wagonjwa 1,537 kwa kusimamisha moyo, kwa mafanikio makubwa huku vifo vikiwa ni 6% tu sawa na wagonjwa 92 kitu ambacho kinawashawishi nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Malawi, Burundi na DR Congo kuleta wagonjwa wao kwenye taasisi hiyo.
“Katika kipindi cha miaka minne huduma za JKCI zimeweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 86 kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 5,744 ambao wangeenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na uwepo wa vifaa vyenye uwezo mkubwa, hususani kwenye masuala ya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo.”
JKCI ni hospitali kuu maalum kwa ajili ya matibabu ya moyo inayomilikiwa na serikali. Ilianzishwa Septemba 2015, na imeendelea kuitangaza vyema nchi yetu hata katika nje ya mipaka yetu.