Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema chanjo ya UVIKO-19 inaendelea kutolewa kwa wananchi ambapo mpaka sasa Watanzania zaidi ya laki tatu wameshapata chanjo hiyo.
Msigwa ameongeza kuwa Serikali inajiandaa kuhakikisha inatenga muda kwa ajili wiki ya kuchanja ili kurahisisha upatikanaji wa chanjo hiyo.
“Kampeni kubwa inayofanyika sasa ni kupeleka chanjo vijijini ili Watanzania wengi waweze kuipata.
“Mwishoni mwa mwezi Septemba au mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu tutakuwa na wiki ya Uchanjaji ambapo viongozi wetu wa nchi nzima watapata chanjo,” amesema Msigwa.
Kuhusu huduma za Posta Msigwa amesema mpango uliopo kwa sasa ni kulipa Shirika la Posta Tanzania nguvu na ufanisi mkubwa zaidi ili liboreshe huduma zake na kuanzisha duka la posta la mtandaoni.
“Shilingi Bilioni 49 zimewekezwa na Serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ubora na kwa haraka zaidi,” amesisitiza Msigwa.
Pia amebainisha kuwa katika mageuzi makubwa ambayo Serikali imeyafanya kwenye Shirika la Posta ni pamoja na mkakati wa kuwa na maduka ya mtandaoni ambapo Watanzania wataweza kuagiza bidhaa na kutuma vifurishi duniani.