Serikali kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye mahakama

0
540

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Augustine Mahiga amesema kuwa ili kuondoa mlundikano wa kesi katika  mahakama mbalimbali nchini,  serikali inaimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA) katika utoaji huduma.

Akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma makadirio ya Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Waziri Mahiga amesema  kuwa matumizi ya TEHEMA yatarahisisha usikilizwaji wa mashauri na kupunguza msongamano wa mahabusu katika magereza.

Akiwalisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria,  Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohamed Nchengerwa ameiomba serikali kufanya maboresho katika sheria za mahakama ili kurahisisha utendaji wa mahakama hizo, huku Msemaji wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni Salome Makamba akishauri kufanyika kwa marekebisho kwa vifungu kadhaa vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nao baadhi ya Wabunge waliopata fursa ya kuchangia makadirio ya bajeti ya wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha wa  2019/2020, wameiomba serikali kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu pamoja na uvunjwaji wa haki za binadamu

 Wizara ya Katiba na sheria imeomba kupatiwa zaidi ya Shilingi  Bilioni 180 ili iweze kutekeleza shughuli zake mbalimbali kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.