Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema wizara yake inafuatilia malalamiko ya wadau wa tasnia ya habari juu ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusabilo Mwakabibi kuwaweka chini ya ulinzi Waandishi wa habari Aprili 12, 2021 mkoani Dar es salaam.
“Tunaomba wanahabari wawe na subira wakati ‘allegations’ [tuhuma] hizi za kusikitisha zinafanyiwa kazi,” amesema Waziri Bashungwa
Mapema jana taarifa zilisambaa mtandaoni kuhusu waandishi wa habari Christopher James wa ITV na Radio One na Dickson Billikwija wa Island TV kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi takribani saa tatu kwa maagizo ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusabilo Mwakabibi.
Inadaiwa kuwa kulikuwa na kikao ambacho Mkurugenzi huyo alikiitisha na wafanyabiashara kutoka Soko la Mbagala Rangi Tatu kisha wafanyabiashara hao waliwaita wanahabari hao ambao walifika hapo kutekeleza majukumu yao kitendo ambacho huenda kilimkera mkurugenzi huyo hivyo akaamuru askari kuwaweka chini ya ulinzi mpaka wamalize kikao kwa hatua zaidi.