Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza Kuwa serikali yake itaendeleza miradi yote mikubwa ya maendeleo ambayo ilianza kutekelezwa katika utawala wa awamu ziliyopita.
Akuhutubia katika sherehe za mwaka mpya 2022 kwa mabalozi mapema leo ikulu, amesema, miradi hiyo ni barabara, reli, usafiri wa angani na majini na mradi mkubwa wa kufua umeme ambapo baadhi ya miradi hii imepata uungwaji mkono mkubwa na mataifa mbalimbali.
Ameainisha maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika usambazaji umeme vijijini ambapo mpaka kufikia mwezi disemba 2021 asilimia 70.1 ya vijiji vyote Tanzania vilikuwa vimeshafikiwa na nishati ya umeme ambapo malengo ni kuongeza asilimia mpaka 78.4 kabla ya mwezi June 2022.
Pia Rais Samia amesema serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege moja ya mizigo na pia vyombo nane vya usafiri majini ambavyo vitagawanywa sawa pande zote za muungano kuendeleza Kazi ya uchumi wa buluu.
Pia Rais Samia ameainisha Kuwa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambalo litakuwa chanzo kikubwa cha nishati katika nia ya nchi ya kuendeleza viwanda umefikia aslimia 53.2.
“Ninaweka umakini mkubwa kwenye mradi huu si tu kutokana na faida zake Kiuchumi, Bali pia kwa mchango wake wa uhifadhi wa mazingira.” Amesema Rais Samia.
Katika hotuba hiyo Rais Samia amesema serikali yake itaendelea kuunga mkono jitihada za balozi zote kuhamia Dodoma baada ya kupatiwa maeneo ya ujenzi na pia kuwataka kuendeleza uwekezaji katika mji huo mkuu wa nchi.