Serikali imedhamiria kuendelea kuwasaidia Wafanyabiashara wa Kitanzania kupitia mafunzo mbalimbali, ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Beng’i Issa, mara baada ya kukabidhi tuzo kwa vijana waliofanya vizuri katika mafunzo ya mtaji mbegu.
Amesema nguvu kubwa imeelekezwa katika kuwajengea Watanzania uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara zao.
“Vijana fursa zipo nyingi mikononi mwenu, na Serikali yenu ipo kwa ajili ya kuwashika mkono mtoke hapo mlipo kuwa juu zaidi, hivyo jitambueni na muongeze ubunifu katika yale mnayoyafanya,” amesema Katibu Mtendaji huyo wa NEEC.
Baadhi ya Wadau walioshirki hafla ya utoaji wa tuzo hizo wamesema kuwa, Vijana wana nafasi kubwa ya kubadili changamoto kuwa fursa, hivyo ni vema wakatambua nafasi waliyonayo katika jamii inayowazunguka.
Baadhi ya vijana waliopata tuzo kutokana na kubuni kibiashara kupitia nishati jadidifu wamesema kuwa, tuzo walizopata zitakuwa chachu ya wao kufanya kazi kwa bidii, na hivyo kukuza biashara zao.
Katika hafla hiyo, vijana 8 kati ya 40 ambao wameonesha ubunifu baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali wamezawadiwa vitendea kazi.