Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini wakiwemo wenye viwanda vya kuzalisha saruji.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Tanga wakati akizungumza na watumishi wa kiwanda cha saruji cha Simba alipotembelea kiwanda hicho, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Amesema kuwa katika kuhakikisha inalinda viwanda vya ndani vya kuzalisha saruji, serikali imeamua kuzuia uingizwaji wa saruji kutoka nje ya nchi.
Majaliwa ameongeza kuwa licha ya serikali kupata kodi kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, pia kiwanda hicho kimesaidia katika kutatua changamoto ya ajira hasa kwa vijana.
Naye Waziri wa Madini, Doto Biteko ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuzingatia sheria zote za madini ukilinganisha na viwanda vingine.
Kiwanda hicho cha saruji cha Simba kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.25 kwa mwaka, lakini kutokana na mahitaji ya soko kinazalisha tani milioni 1.075 kwa mwaka.