Serikali kuendelea kushirikiana na madhehebu ya dini

0
2236

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini katika kuwaletea Watanzania maendeleo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa sherehe za kusimikwa wakfu Askofu Mkuu Msaidizi pamoja na Maaskofu wanne wa majimbo wa Kanisa la Pentekoste Motomoto,- Mwanga mkoani Kigoma.

“Serikali imeweka mazingira rafiki kwa madhehebu ya dini nchini kuweza kutoa huduma za kijamii hususan elimu na afya” amesema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kanisa kujiepusha na migogoro ya kiutawala ndani ya Kanisa na pia liepuke kuchanganya dini na siasa.

“Kazi kubwa ya Kanisa iwe kuhubiri amani kwa waumini wake na wananchi kwa jumla” amesema Makamu wa Rais huku akinukuu neno la Mungu katika Waebrania 12:14 ambalo linasema “tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote”.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza kuwa eneo jingine ambalo serikali inalitegemea Kanisa ni katika kujenga maadaili mema ya jamii, hivyo ameliomba Kanisa hilo kusaidiana na serikali katika kupiga vita tamaduni zisizofaa ili kujenga Taifa lenye maadili ya Kitanzania.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo la Pentekoste Motomoto,- Mwanga mkoani Kigoma, -Ezra Mtamya ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kuijenga Tanzania yenye maendeleo na kwamba kama Kanisa wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya jamii na utunzaji wa mazingira.

Ameiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kuwapatia wataalam wa mazingira pamoja na wale wa ufugaji nyuki ili waweze kuwaelekeza njia bora za utunzaji wa mazingira na ufugaji nyuki.