Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ili wawekeze kwenye ujenzi wa viwanda na hivyo kukuza uchumi wa Taifa na kuongeza ajira.
Akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Sikonge mkoani Tabora wakati wa uzinduzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda yenye urefu wa kilomita 342.9 inayounganisha mkoa wa Tabora na Katavi, Rais Samia Suluhu Hassan amesema barabara hiyo itachochea shughuli za uzalishaji na usafiri katika mikoa hiyo.
Amesema serikali imeendelea kuvutia wawekezaji kuwekeza nchini, ambapo kiwanda cha Tumbaku cha Morogoro kimepata mwekezaji ambaye ameanza taratibu za kukifufua.
Pia amewataka wakulima wa Tumbaku kuongeza uzalishaji, kwa kuwa kuna uhakika wa soko la bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, mwekezaji mwingine ameshaanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea mkoani Dodoma ambapo sasa wakulima watapata mbolea hapa nchini tofauti na awali mbolea zote zilikuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa mbolea mwaka huu.