Serikali kuendelea kuhamasisha matumizi.ya kiswahili

0
133

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amezitaka wizara zenye dhamana ya elimu kufanyia kazi matokeo ya tafiti ambazo zimefanyika kuhusu lugha ipi inafaa kufundishia, ili serikali ifanye uamuzi na hatimaye watoto wa Kitanzania waanze kujifunza kwa lugha ya kiswahili kuanzia shule ya awali hadi Chuo Kikuu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Ametoa wito kwa wataalam na mabingwa wa lugha ya Kiswahili kuendelea kuongea kiswahili fasaha pamoja na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali kwa lugha hiyo, ili kuendelea kukabiliana na ongezeko la upotoshaji wa matumizi ya lugha ya kiswahili miongoni mwa jamii.

Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali, kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili na kujenga ushawishi kwa nchi nyingine kuingiza Kiswahili katika mitaala yao ili kuendelea kusambaza lugha hiyo adhimu.

Awali akisoma salamu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa upande wa Tanzania , mkuu wa kitengo cha elimu kutoka shirika hilo Faith Shayo amesema, kuthamini lugha mbalimbali ni kipaumbele cha shirika hilo.

Amesema Kiswahili ni kati ya lugha kumi zinazozungumzwa sana duniani, na kujenga utengamano miongoni mwa jamii na mataifa mbalimbali.