Serikali kuboresha mazingira ya kazi ya waandishi wa habari

0
149

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali imejidhatiti kujenga mazingira bora ya wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru ikiwa ni pamoja na kupata haki zao stahiki kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Waziri Nape ametoa kauli hiyo wakati wa ibada ya kuaga miili ya waandishi wa habari waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari mkoani Mwanza.

Amesema kazi ya serikali ni kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri ya wanahabari kufanya kazi kwa uhuru  na kuepusha madhara makubwa yanayoweza kuwakumba wakiwa wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi mapana ya taifa.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa wanahabari kwa kufanyia kazi marekebisho ya sheria inayosimamia tasnia ya habari kwani bila wao kazi zinazofanywa na Serikali zisingeonekana.

“Rais Samia Suluhu Hassan alishaagiza tupitie mapungufu yaliyomo kwenye sheria ya habari hivyo tutayafanyia kazi kwa wakati muafaka ili kukidhi matarajio ya wanahabari,” amesema Nnauye.

Kwa upande wake Mkuu wa  Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel  amesema waandishi wa habari walioaga dunia wamefia taifa lao kwa kutumia kalamu zao hivyo kuwapoteza ni pigo kubwa kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla.

Shughuli ya kuaga miili ya waandishi habari imefanyika katika uwanja Nyamagana Mwanza huku ikihudhuriwa na viongozi mbalimbi ya Serikali, viongozi wa dini pamoja na wananchi.