Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema Serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Msomera ambao unaendelea na shilingi milioni 50 kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za afya katika zahanati ya kijiji cha Msomera katika kata ya Misima wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga inayotoa huduma kwa wananchi wasiopungua elfu 10.
Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaongeza watumishi ambao ni wauguzi, wataalam wa maabara na dawa ili ukarabati unaofanyika uendane na huduma nzuri zinazoendelea kutolewa hapo.
Vile vile, amesema Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Nchini (TARURA) unaendelea na ujenzi wa barabara inayotoka Handeni Mjini hadi kata ya Misima kwa kujenga makalavati na boksi kalvati katika maeneo korofi.
Pia, amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupeleka fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa awali ili yaweze kuwahudumia watoto wadogo walio katika eneo la Msomera.