Rais Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya serikali ni kufikisha maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafikishia huduma muhimu za umeme na maji.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo Ikulu mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na viongozi na wadau mbalimbali wa nishati mara baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba ya miradi ya Uimarishaji Gridi ya Taifa na Umeme Vijijini.
Amesema kazi ya kuwapelekea maendeleo wananchi hasa umeme bado ni kubwa, kwani ni asilimia 43.9 tu ya vitongoji nchini ndivyo vina huduma ya umeme.
Miradi ambayo mikataba yake imesainiwa hii leo ni 26 na ina thamani ya shilingi trilioni 1.9.
Dkt. Samia amesema mikataba hiyo iliyosainiwa baina ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijinini (REA) pamoja na wakandarasi mbalimbali utanufaisha maeneo 336 ya uzalishaji, hivyo ina faida kubwa kwa Watanzania kwa kuwa itahusisha pia migodi midogo, kilimo, vituo vya afya na vyanzo vya maji.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kilio kikubwa cha hivi sasa cha Watanzania wengi ni umeme na kwamba serikali imepokea kilo hicho na itahakikisha suala hilo linashughulikiwa.