Serikali imeanza mazungumzo na nchi za Misri na Algeria ili kuuza Tumbaku ya Tanzania

0
4316

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeanzisha mazungumzo na nchi wanachama wa COMESA na nchi kama Misri na Algeria kupitia balozi zake ili kuandaa Makubaliano Maalum (Bilateral Agreement) yatakayoiwezesha Tanzania kupeleka tumbaku kwa kodi nafuu.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 17 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mhe Edwin Amandus Ngonyani Mbunge wa Namtumbo aliyetaka kufahamu Wizara ya Kilimo inashirikianaje na Wizara nyingine zinazohusika na uwekezaji wa mambo ya nje kutafuta soko la tumbaku nchini Misri badala ya kulazimika kutumia nchi za Uganda na Kenya pekee.
Mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri na matarajio ni kufungua milango ya soko hilo na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na taifa kwa ujumla. Aidha, Makubaliano hayo yakikamilika Tanzania inaweza pia kuuza chai nchini Misri na Algeria kwa faida kuliko ilivyo hivi sasa au badala ya kuuza chai kupitia mnada wa Mombasa nchini Kenya.