Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali haitavumilia tabia ya wafanyabiashara wachache wenye dhamira ovu ya kuwaumiza wananchi kwa kujiamulia kupandisha bei za bidhaa bila kufuata utaratibu kwa manufaa yao binafsi kwa kuwa Serikali inajukumu la msingi la kusimamia ushindani wa haki kwenye soko kwa kudhibiti mienendo hadaifu au kandamizi ya wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara wanaopandisha holela wa bei za bidhaa nchini.
Waziri Kijaji ameyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya uchunguzi uliofanywa na FCC, kuhusu uhaba na kupanda kwa bei za vinywaji baridi uliotokea Oktoba hadi Januari 2022 ulitokana na kutopatikana kwa sukari ya viwandani kwa sababu ya ukosefu wa Makasha ya kusafirishia shehena ya sukari hiyo kuja hapa nchini uliojitokeza duniani kote.
Aidha Waziri kijaji amewahakikishia watanzania kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa Sukari hiyo ya viwandani inapatikana kwani hadi sasa tani 25,000 ya sukari ya viwandani imeingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam na inaendelea kupokelewa kwa kuwa Sukari hiyo kwa sasa inasafirishwa kwa njia ya mbadala ya ufungashaji shehena usiotumia makasha (containers), yaani break-bulk.
Akielezea hatua nyingine ambazo Serikali imechukua ili kutatua changamoto hiyo, Waziri Kijaji amezielekeza Mamlaka na Taasisi za Serikali zikiongozwa na Tume ya Ushindahi (FCC) zilizopewa dhamana ya kusimamia mienendo ya masoko ya bidhaa kutekeleza wajibu huo kikamilifu na kwa umakini mkubwa ili kudhibiti mienendo hadaifu au kandamizi ya wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara kwenye soko ikiwa ni pamoja na upandishaji holela wa bei za bidhaa nchini.
Aidha, Waziri Kijazi amewaelekeza Maafisa Biashara wa Mikoa kote nchini waendelee kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye maeneo yao na kuwasilisha taarifa hizo mara kwa mara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Pia Waziri Kijaji amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuongeza ufanisi katika uondoshaji wa shehena bandarini, kuboresha usafirishaji kwenye barabara kuu na kuimarisha upitishaji wa mizigo mipakani kwa kuwa imeanzisha mfumo wa utoaji wa vibali vya kuagiza sukari ya viwandani kwa njia ya mtandao ili vibali hivyo vipatikane kwa wakati na bila usumbufu wowote.
Dkt. Kijaji pia amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na kuwekeza nchini kwa lengo la kujenga uchumi imara wa viwanda ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa sukari ya viwandani hapa nchini ili kuondoa utegemezi wa kuagiza sukari hiyo kutoka nje.