Taasisi ya Kimataifa ya World Travel Awards imetangaza hifadhi mbili za Tanzania kuwa washindi katika vipengele vya hifadhi Bora na kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imetangazwa kuwa mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora Barani Afrika (“Africa’s Leading National Park 2024”) wakati Mlima Kilimanjaro ukitangazwa kuwa Kivutio bora cha Utalii Barani Afrika (African Leading Tourist Attraction 2024).
Taarifa iliyotolewa na Afisa Mhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Catherine Mbena, imesema tuzo hizo zimetolewa usiku wa kuamkia leo (Oktoba 18, 2024) katika Ukumbi wa Hotel ya Diamonds Leisure Beach & Golf Resort ya nchini Kenya.
Akitangaza washindi, Mwanzilishi wa Taasisi ya World Travel Awards, Graham Cooke amesema kuwa Serengeti imezishinda hifadhi zingine kwa ubora barani Afrika ambazo ni Maasai Mara ya nchini Kenya, Kruger ya Afrika Kusini, Central Kalahari ya Botswana, Etosha ya Namibia na Kidepo Valley ya nchini Uganda.
Cooke amesema kuwa Mlima Kilimanjaro pia umevishinda vivutio vingine vya utalii barani Afrika ambavyo ni hifadhi ya Ngorongoro (Tanzania), Hartbeespoort aerial cableway, V& A Waterfront, Robben Island, Table Mountain (zote za Afrika Kusini), Ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana, na Pyramid of Giza ya Misri.
Tuzo hizo zimepokelewa na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula. Wengine katika ujumbe huo ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii, Ephraim Mafuru, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, CPA Hadija Ramadhani, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrita Lyimo pamoja na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Stephano Msumi.
Ushindi huu wa Kishindo wa Serengeti katika kipengele cha Hifadhi Bora barani Afrika ni wa mara ya sita mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi sasa 2024.
Kwa mujibu wa Catherine Mbena, ushindi wa mwaka huu pamoja na jitihada zingine, umechagizwa na kampeni ya TANAPA ya ‘Vote Now’ iliyofanyika kwa miezi mitatu mfululizo.
Kwa upande wa Mlima Kilimanjaro, Catherine amesema katika taarifa kwamba na umeshinda tuzo ya kivutio Bora Barani Afrika kwa mara ya sita ingawa si mfululizo kwani ulishinda mwaka 2013, 2015, 2016, 2017, 2018, na sasa 2024.