Sekta binafsi ni mhimili wa maendeleo

0
231

Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) amesema sekta binafsi ni mhimili muhimu wa maendeleo ya nchi kwasababu huchangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi.

Rais amesema hilo mapema leo alipoongoza mkutano wa 12 wa baraza hilo lililojadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya kodi, mamlaka za udhibiti pamoja mazao yatokanayo na misitu.

Katika mkutano huo amesisitiza kuwa hakuna Taifa lolote duniani ambalo linaweza kupiga hatua ya maendeleo bila kushirikiana na sekta binafsi, hivyo amewaagiza mawaziri wa sekta mbalimbali kukaa na kujadiliana na wafanyabiashara wa sekta binafsi ili kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili.

Aidha, Rais amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni Wenyeviti wa Mabaraza hayo katika ngazi za Mikoa na Wilaya kushirikiana na Sekretarieti ya Baraza Taifa na kuhakikisha Mabaraza hayo yanafanyika kwani ndio chimbuko la mabadiliko katika ngazi ya Taifa.