Sekretarieti ya Ajira yaendelea kupokea maombi

0
989

Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imepokea jumla ya maombi 594,300 kutoka kwa waombaji wa nafasi za kazi katika Utumishi wa Umma zilizotangazwa kwenye Wizara, Idara, Wakala, Sekretarieti za mikoa, manispaa, halmashauri na Taasisi za umma kuanzia mwezi Novemba  mwaka 2015 hadi hivi sasa.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka mitatu ya Sekretarieti hiyo kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka huu jijini Dar es salaam, Katibu wa Sektretarieti ya Ajira, – Xavier Daudi amesema kuwa tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya Tano, serikali imetangaza nafasi zilizo wazi 6,554 ambapo jumla ya waombaji Laki Moja na Elfu Arobaini waliitiwa katika usaili.

Xavier ameongeza kuwa hadi kufikia Disemba 15 mwaka huu,  jumla ya nafasi za wazi za kazi 6,099 zilikwishajazwa, huku nafasi 455 zilizotangazwa kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu mchakato wake ukiendelea na utakamilika hivi karibuni.

Ameongeza kuwa mbali na mchakato huo, pia wapo watumishi walioajiriwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kada za Afya na Ualimu, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya watumishi wa kada za afya 24,728 wameajiriwa wakati kwa upande wa kada ya ualimu jumla ya walimu 40,086 waliajiriwa serikalini.

“Idadi hii inaweza kuongezeka katika mwaka huu wa fedha wa  2018/2019 kwa watumishi watakaoajiriwa katika kada za walimu, afya pamoja na watumishi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama ambao utaratibu wake wa ajira unataratibiwa na mamlaka husika” amesema Katibu huyo wa Sektretarieti ya Ajira nchini.

Akizungumzia udhibiti wa waombaji wasio na sifa ikiwemo wenye vyeti vya kughushi, Xavier amesema kuwa Serikali  hiyo ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeendelea kukagua  nyaraka za waombaji mbalimbali vikiwemo vyeti vyao ili kuhakikisha kuwa wanaoajiriwa ni wale wenye sifa na vyeti vinavyostahili kwa mujibu wa sheria.

Akifafanua zaidi,  Xavier amesema kuwa kati ya mwaka 2015 na 2018,  jumla ya nyaraka za vyeti vya waombaji kazi 18,817 viliwasilishwa kwenye mamlaka zinazohusika na utoaji wa vyeti hivyo kwa ajili ya uhakiki, ambapo vyeti halali vilikuwa 18,112 na vyeti 706 vilibainika kuwa ni vyeti vya kughushi.