“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha mtangazaji maarufu na mahiri Ndg. Marin Hassan kilichotokea leo asubuhi Jijini Dar es Salaam. Marin Hassan aliipenda kazi yake ya uandishi wa habari, aliifanya kwa weledi wa hali ya juu, alikuwa mzalendo wa kweli na alidhamiria kuitumikia nchi yake kupitia chombo cha habari cha Taifa (TBC) kwa nguvu na juhudi zake zote”.
Hii ni sehemu ya salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa kufuatia kifo cha Mwandishi wa Habari Mwandamizi na mtangazaji maarufu wa Shirika la Utangazji Tanzania (TBC) Bw. Marin Hassan Marin kilichotokea leo asubuhi tarehe 01 Aprili, 2020 katika Hospitali ya Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ametoa pole kwa familia ya Marin Hassan, Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba, Wafanyakazi wote wa TBC, Waandishi wa Habari wote na wote walioguswa na kifo cha mwanahabari huyo nguli hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amesema alimfahamu Marin Hassan kama mtu aliyetoa mchango mkubwa katika ustawi wa Uandishi wa Habari nchini Tanzania na kwa juhudi zake kubwa ndani ya TBC ambapo aliliripoti habari kwa ubunifu na mvuto wa hali ya juu, alibuni na kufanya vipindi vilivyopendwa na Watanzania ikiwemo vipindi vya Uchaguzi Mkuu, Safari ya Dodoma na mabadiliko makubwa yaliyoanza juzi ambapo TBC inatangaza habari zake kupitia ARIDHIO.
“Marin Hassan ameondoka wakati ambapo tunamhitaji zaidi, Marin Hassan ni shujaa wa habari Tanzania, aliipenda sana TBC na nchi yake Tanzania. Naungana na familia yake, TBC na Waandishi wa Habari wote kumuombea apumzike mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli. Inna Lillahi wa inna ilayhi raji’un
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
01 Aprili, 2020