Sagini: Mkakati wa kumaliza ajali waja

0
128

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amesema, baraza hilo limeandaa mkakati utakaomaliza ama kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani.

Naibu Waziri Sagini ameongeza kuwa mkakati huo utadhibiti uendeshaji wa vyombo vya moto pamoja na madereva ambao mara kadhaa wamekuwa chanzo cha ajali za barabarani hapa nchini.

Akitoa taarifa ya Baraza hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Sagini amesema, mkakati huo utakuja na udhibiti wa madereva wanaotumia kilevi na kuendesha vyombo vya moto na udhibiti wa mwendokasi kwa madereva.

Mkakati mwingine ni kuwashirikisha wamiliki wa magari ikiwa ni pamoja na kuweka madereva wenza kwa mabasi yanayokwenda masafa marefu, kudhibiti uendeshaji magari bila sifa na kudhibiti uendeshaji magari bila bima.

Naibu waziri Sagini amesema mkakati huo utadhibiti usafirishaji wa abiria kwa magari madogo yenye gurudumu moja, kudhibiti uendeshaji wa pikipiki na bajaji na kufunga mikanda wakati wote wawapo safarini.