Royal Tour yalikosha Shirikisho la Michezo ya Majeshi Duniani

0
1153

Balozi wa Shirikisho la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM), Kanali Dorah Mamby ambaye ni Mwambata Jeshi nchini Guinea amesema kupitia kazi iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya Uzinduzi wa Filamu ya Tanzania: The Royal Tour, mataifa wanachama wa shirikisho hilo yanatamani kuiona Tanzania ikiandaa Mkutano Mkuu wa CISM ili kuyapatia fursa adhimu ya kuitembelea nchi ya Tanzania.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam katika ofisi za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , katika ziara yake nchini Tanzania yenye lengo la kuitambulisha CISM kwa mamlaka za juu za Serikali ili kuyawezesha majeshi kushiriki mashindano ya shirikisho hilo katika michezo ya Gofu, mpira wa miguu, ndondi na riadha.

Amesema katika ziara yake amepata fursa ya kutoa heshima kwenye mnara wa mashujaa wa vita vya ukombozi wa Taifa la Tanzania, pia ametembelea Makumbusho ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Visiwa vya Zanzibar ambapo huko alivutiwa na hifadhi ya urithi wa kihistoria ambao ulimwengu hususani wanachama wa CISM wanatakiwa kuufahamu.

Aidha, ameongeza kuwa  kupitia  fursa hiyo ya kufanya ziara nchini Tanzania, yeye kama Raia wa nchi ya Guinea, anatambua urithi wa tunu za uzalendo na ushikamano zilizoachwa na marais waliopita wa nchi ya Tanzania na Guinea.

Akimtaja Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sekou Toure kama viongozi waliotangalia wa nchi hizo amesema kutokana na urithi ulioachwa na viongozi hao, kilianzishwa chuo kikuu kifahamikacho kwa jina la Mwalimu Julius Nyerere huko Kankan Guinea ambapo yeye ni mmoja wa wanafunzi waliosoma chuoni hapo.