Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya uchunguzi wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kutoka kwa kamati iliyoundwa na serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo.
Waziri Mkuu amepokea ripoti hiyo jijini Dar es salaam aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu Jenerali George Waitara.
Mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ameishukuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais John Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.
Pia ameipongeza kamati hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa serikali juu ya mambo waliyoyabaini.
“Nimepokea taarifa kwa niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa kazi,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika ripoti hiyo ni yale ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi.
Kivuko cha MV Nyerere kilipinduka na kuzama Septemba Ishirini mwaka huu katika ziwa Viktoria ambapo zaidi ya watu Mia Mbili walikufa maji na wengine zaidi ya arobaini kuokolewa.
Kufuatia ajali hiyo, Septemba 24 mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa alitangaza kamati ya kuchunguza ajali hiyo, Kamati yenye wajumbe saba na kuitaka kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.