Ripoti ya CAG yaanika madudu bandari ya Kigoma, Waziri Mkuu ageuka Mbogo

0
302

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Tanga na Kyela kutokana na kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
 
Waziri Mkuu Majaliwa pia amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Nuru Mhando na Meneja wa Matumizi ya Fedha wa TPA,- Witness Mahela ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazowakabili.
 
Amechukua hatua hiyo baada kupokea ripoti ya ukaguzi Maalum uliofanywa na CAG katika hesabu za bandari ya Kigoma kwa mwaka 2017/2018 na mwaka 2018/2019 ambapo lengo la ukaguzi huo lilikuwa kujiridhisha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.
 
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jijini Dar es salaam katika kikao chake na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania na Menejimenti ya TPA, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania ( TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI).

Amesema TPA imebeba taswira ya uchumi wa Taifa, hivyo lazima kazi ifanyike vizuri na kuitaka Bodi ya TPA kuhakikisha Mamlaka hiyo inafanyakazi kwa weledi na isisite kuchukua hatua kwa mtumishi atakayebainika kutenda makosa.
 
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, miongoni mwa mambo yasiyoridhisha yaliyofanywa na TPA na kuikosesha serikali mapato, ni kutoa msamaha wa kodi ya zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa kiwanda cha saruji cha Mbeya licha ya kukataliwa na kamati ya misamaha.
 
Amesema licha ya kuongezeka kwa makusanyo katika Bandari, lakini kati ya fedha inayokusanywa ni asilimia 70 tu ndiyo inayoingia Serikalini na kiasi kilichobaki kinaishia mifukoni jambo ambalo halikubaliki.

”Ripoti ya CAG ya Bandari ya Kigoma haijatufurahisha imeonesha mambo mengi mabovu.”amesisitiza Waziri Mkuu.
 
Amesema katika hali isiyokuwa ya kawaida, TPA iliidhinisha malipo ya shilingi bilioni 8.2 kwenda bandari ya Kigoma kwa ajili ya kufanya malipo mbalimbali huku ukomo wa bandari hiyo ni shilingi bilioni 7.4 na kwamba fedha hizo zilitumika kufanya malipo yasiyostahili kwa watu mbalimbali akiwemo mfanyabiashara wa duka la ujenzi mjini Kigoma, – Eliya Mtinyako aliyelipwa zaidi ya shilingi milioni 900.
 
“Malipo haya yamefanyika huku kukiwa hakuna nyaraka zinazoonesha kama alilipwa kwa sababu zipi kwani mfanyabiashara huyo aliyelipwa hakuwahi kutoa huduma yoyote kwa mamlaka hiyo na wala si mzabuni. Pia amelipwa bila ya kuwepo kwa nyaraka za madai.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Amesema licha ya upotevu huo wa fedha katika bandari hiyo ya Kigoma, pia Mhasibu wa Bandari ya Kigoma, Madaraka Madaraka alifuta madeni ya zaidi ya shilingi bilioni moja waliyokuwa wakidaiwa wateja bila ya kufuata taratibu.