Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge amewasisitiza wananchi kufanya mazoezi na kuepuka ulaji usiofaa ili kujikinga na magonjwa yasiyo ambukiza ikiwemo shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, saratani na kisukari ambayo yamekuwa chanzo cha vifo na usumbufu kwa wananchi.
RC Kunenge amesema hayo wakati wa ufunguzi wa wiki ya kitaifa ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza inayoanza Novemba 07 hadi 14 kwenye viiwanja Mnazi Mmoja ambapo amesema katika wiki hiyo wananchi watapata fursa ya kupimwa magonjwa mbalimbali bure na kupatiwa ushauri wa kitaalamu.
Aidha, amesema kwa kuwa magonjwa hayo yanaweza kuzuilika ni vyema wananchi wakaanza kuchukuwa tahadhari mapema kwa kuhakikisha wanazingatia ulaji bora, kupunguza ulevi usiofaa, kupunguza uvutaji wa sigara na kuzingatia michezo.
Pamoja na hayo RC Kunenge amesema serikali itaendelea kutoa elimu ya kutosha ya namna bora ya kukabiliana na magonjwa hayo na kuendelea kuboresha na kuongeza miundombinu mbalimbali ya afya.
Ufunguzi wa maadhimisho hayo umehusisha watendaji kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mashirika na asasi za kiraia na yameenda sambamba na matembezi pamoja na mechi za kirafiki kati ya timu ya Azam na ofisi ya mkuu wa mkoa pamoja na timu nyingine.
Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali za kitabibu duniani, magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakichangia vifo vingi vya watu kutokana na jamii nyingi kutojua namna ya kujikinga au kukabiliana nayo.