RC Kunenge awapa ‘Tano’ wauguzi kwa kazi wanayoifanya

0
248

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amewapongeza wauguzi wa mkoa huo, kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya katika kuokoa maisha ya wananchi jambo linalosaidia kupunguza vifo.

Kunenge amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi mkoa wa Dar es salaam, ambapo amewahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa uwezo wao wote na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega.

Aidha Kunenge amesema Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za Afya kupitia ujenzi wa hospital, zahanati, vituo vya Afya na kununua vifaa tiba ili kuhakikisha wanatatua kero za wananchi.

Pamoja na hayo amesema anafurahi kuona hata zile kelele za wananchi, kuhusu lugha chafu zimepungua na badala yake sasa hivi wauguzi wamekuwa na lugha za upendo kwa wagonjwa jambo linalotia faraja.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rashid Mfaume amewaalika wananchi kujitokeza kwenye viwanja vya Karimjee kujionea kazi zinazofanywa na wauguzi wa mkoa huo.

Aidha Dkt. Mfaume amewaahidi wananchi kutegemea mabadiliko makubwa katika sekta ya afya kwa kuwa Serikali ya mkoa imejidhatiti vizuri kutoa huduma bora na zenye tija.