RC Kunenge afanya ziara ya kushtukiza usiku wa manane, Atoa maagizo kwa wakandarasi wazembe

0
287

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amefanya ziara ya kustukiza usiku wa manane kwenye miradi mitatu mikubwa ikiwemo ya ujenzi wa machinjio ya kisasa Vingunguti, Soko la Kisutu na ujenzi wa Stendi ya kisasa Mbezi Louis kujionea kama agizo alilotoa la kufanya kazi usiku na mchana linatekelezwa.

Akiwa kwenye ujenzi wa Machinjio ya kisasa Vingunguti na Soko la Kisutu RC Kunenge amekuta agizo la kufanya kazi usiku na mchana halijatekelezwa, jambo linalopelekea miradi hiyo kushindwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa na kuleta kero kwa wananchi.

Kutokana ukiukwaji wa maagizo yayo RC Kunenge, ametoa maagizo matatu mazito kwa Manispaa ya Ilala ikiwemo kuhakikisha mkandarasi anapigwa faini kwa kushindwa kukamilisha ujenzi ndani ya muda kwa mujibu wa mkataba, kumchukulia hatua za kinidhamu msimamizi wa Mradi pamoja na kumuwajibisha mhandisi Manispaa hiyo kwa kushindwa kusimamia kazi yake.

Aidha RC Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kumpatia mapendekezo ya jinsi gani watakamilisha miradi hiyo kwa haraka ili iweze kuwa msaada kwa wananchi.

Pamoja na hayo RC Kunenge ametembelea ujenzi wa Stand Mpya ya Mbezi Louis na kukuta kazi inafanyika usiku na mchana ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilotoa wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi na kuagiza mradi ukamilike kabla ya mwishoni mwa mwezi Novemba.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa taasisi zote za Serikali zinazohusika kufanikisha miradi kuhakikisha wanafanya kazi kwa kushirikiana ili miradi iweze kukamilika kwa wakati.