Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti leo amezindua chanjo ya UVIKO-19 huku akiwata wananchi wa Mtwara kuendelea kuzingatia taratibu zote za kujikinga na ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
Gaguti amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuruhusu Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimepata chanjo ya UVIKO-19 na leo imeanza kutolewa kwa wananchi.
Amesema kwa awamu ya kwanza, mkoa huo umepata chanjo dozi 20,000 ambazo zitaanza kutolewa kwa wahudumu wa afya, watu wenye umri kuanzia miaka 50 na watu wenye changamoto za maradhi sugu kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Amesema kuwa mahitaji ya chanjo mkoani humo bado ni mkubwa kwani takribani watu 250,000 mpaka sasa wanahitaji chanjo, huku akiahidi kuhakikisha chanjo zaidi zinapelekwa.
Chanjo ya UVIKO-19 imeanza kutolewa leo kwa Halmashuri ya Mtwara na kesho zitasambazwa katika halmashuri za mkoa kupitia vituo vya Afya.