Ratiba ya uchaguzi mkuu haijatoka: NEC

0
276

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema haijatoa wala kutangaza ratiba yoyote ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2020.

Taarifa iliyotolewa na NEC kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa, utaratibu wa tume ni kupanga ratiba ya uchaguzi mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukio ambalo bado muda wake haujafika.

Ufafanuzi huo wa NEC umetolewa kufuatia kuwepo kwa taarifa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zinazopotosha taarifa ya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

NEC imewaomba wananchi kupuuza taarifa ya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi zinazosambazwa katika mitandao hiyo kwa kuwa si rasmi, na kwamba kitendo hicho kinafanyika kwa nia ovu.

Kwa mujibu wa NEC, ratiba ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu itatolewa muda utakapowadia kulingana na matakwa ya kisheria.